Back

ⓘ Kampeni za Kivita katika Afrika ya Mashariki, Vita ya Kwanza ya Dunia. Kampeni za Afrika ya Mashariki zilikuwa mfululizo wa mapigano ya kivita yaliyotokea Afrik ..
Kampeni za Kivita katika Afrika ya Mashariki (Vita ya Kwanza ya Dunia)
                                     

ⓘ Kampeni za Kivita katika Afrika ya Mashariki (Vita ya Kwanza ya Dunia)

Kampeni za Afrika ya Mashariki zilikuwa mfululizo wa mapigano ya kivita yaliyotokea Afrika ya Mashariki ya Kijerumani na koloni jirani za Msumbiji, Rhodesia ya Kaskazini, Afrika ya Mashariki ya Kiingereza, Uganda, na Kongo ya Kibelgiji. Kampeni hizi zilianza mwezi wa Agosti 1914 zikaisha rasmi mnamo mwezi wa Novemba katika mwaka wa 1918.

                                     

1. Wajerumani na mataifa ya ushirikiano

Wapiganaji katika vita hii walikuwa Schutztruppe jeshi la kikoloni cha Kijerumani lililofanywa hasa na askari Waafrika waliosimamiwa na maafisa Wajerumani pamoja na walowezi Wajerumani na wanamaji wa manowari ya Kijerumani waliokaa Afrika ya Mashariki wakati wa mwanzo wa vita 1914.

Dhidi yao walisimama jeshi dogo la kikoloni la Kiingereza katika Kenya na Rhodesia, halafu vikosi vya jeshi la kikoloni la Uhindi ya Kiingereza na vikosi kutoka Afrika Kusini na Afrika ya Magharibi.Pia walishiriki vikosi vya Force Publique ya Kibelgiji kutoka Kongo. Tangu mwaka 1916 jeshi la kikoloni la Kireno katika Msumbiji liliingia upande wa Uingereza.

Mikakati ya jeshi la kikoloni la Kijerumani lililoongozwa na Luteni Koloneli baadaye Meja-jenerali Paul Emil von Lettow-Vorbeck ililenga kuwalazimisha wapinzani hasa Waingereza kutumia wanajeshi wengi iwezekanavyo katika Afrika kwa shabaha ya kuwazuia wasipatikane kwenye vita ya Ulaya.

Mkakati yake ilifaulu kiasi cha kwamba Waingereza walipaswa kuleta vikosi vikubwa kutoka Uhindi ya Kiingereza na Afrika Kusini kupigania kempeni ya Afrika ya Mashariki, ingawa haikuwa na umuhimu wowote kwa mwendo wa vita pale Ulaya.

                                     

2. Awamu ya kwanza: 1914-1915

Katika awamu ya kwanza ya vita vikosi vya Schutztruppe vilishambulia reli ya Uganda na vituo vya mpakani na Kenya. Waingereza walijibu kwa kukusanya walowezi wao katika Kenya bila kufaulu kuwazuia Wajerumani walioteka mji wa Taveta. Hiyvo Waingereza walichukua askari 12.000 Wahindi na 2 Novemba 1914 walishambulia Tanga. Lakini askari Waafrika wa jeshi la Kijerumani waliwashinda Tanga na baadaye pia Longido karibu na mlima Kilimanjaro, wengine huko Yasini.

Hapo Waingereza waliamua kuchukua wanajeshi Wazungu kutoka Afrika Kusini chini ya amri wa jenerali Jan Smuts waliofika Kenya hadi mwisho wa 1915. Wakati huohuo Wabelgiji walipanga pamoja na Uingereza kupeleka vikosi vya jeshi lake la Force Publique katika Kongo mpakani wa magharibi.

Manowari SMS Königsberg ilikuwa Dar es Salaam wakati wa Julai 1914 ikaondoka bandarini na kushambulia meli za Kiingereza kwenye Bahari Hindi. Waingereza walijaribu kuizuia walituma manowari tatu HMS Astraea, HMS Pegasus na HMS Hyacinth kutoka Afrika Kusini kuelekea Dar es Salaam. SMS Königsberg ilianza kukosa makaa kwa injini yake ikarudi Afrika ya Mashariki; ilipopita Zanzibar ikakuta HMS Pegasus bandarini na kuizamisha. Königsberg ikakimbia ikajificha katika mdomo wa mto Rufiji. Waingereza walikusanya manowari kadhaa mbele ya mto Rufiji; manowari zao zilishindwa kuingia ndani ya mdomo wa mto lakini walivamia kisiwa cha Mafia na kuanzisha kiwanja cha ndege; hatimaye walifaulu kupiga Königsberg mara kadhaa na kusababisha uharibifu mkali hadi nahodha Mjerumani aliamua kuzamisha manowari yake mwenyewe kwenye tarehe 11 Juni 1915. Mabaharia Wajerumani walitoa mizinga yao na kuipeleka kwenye nchi kavu wakajiunga na Schutztruppe.

                                     

3. Awamu ya pili: shambulio dhidi ya Tanganyika

Januari 1916 jeshi hili lilishambulia. Jeshi la Kijerumani lilikuwa ndogo likafuata mikakati ya kuwachelewesha maadui na kuwashambulia walipokuwa wadhaifu au walipofanya makosa.

 • Vikosi kutoka Uhindi, Afrika Kusini na Uingereza vilivamia Tanganyika kutoka upande wa Kenya
 • Wareno walivamia pembetatu ya Kionga nchi ngambo ya mto Rufiji na nyanda za juu za Umakonde. Lakini walishindwa hapa wakapaswa kurudi Msumbiji
 • Wanajeshi 5.000 Waingereza na Waafrika Kusini walivamia kusini magharibi ya Tanganyika kutoka Nyassaland Malawi na Rhodesia Zambia
 • Wabelgiji waliingia Rwanda na Burundi kutoka Kongo wakafuata njia ya reli kuelekea Tabora

Hadi Agosti 1916 mataifa ya ushirikiano yalishika miji muhimu ya Tanganyika isipokuwa Daressalaam. Moshi iltekwa mwezi wa Machi. Reli ya Kati ya Tanganyika kuanzia Tabora, Dodoma hadi Morogoro ilikuwa mkononi mwao. Walisita kuvamia Daressalaam kwa sababu waliogopa mapigano makali lakini Lettow-Vorbeck aliwahi kuondoa askari wake tayari kwa sababu hakutafuta mapigano makubwa dhidi ya maadui mwenye nguvu zaidi. Alipeleka jeshi lake katika eneo upande wa kusini wa mstari Daressalaam-Morogoro-Iringa pasipo na njia nzuri akitegemea Waingereza wasingeweza kutumia usafiri kwa malori na reli.

Hadi hapa maendeleo ya vikosi vya maungano yalikuwa na matatizo mengi. Walitegemea hasa askari Wazungu na Wahindi waliozoea kusafiri na mizigo mikubwa ya vyakula, nguo na hema na kwa hiyo walihitaji wapagazi wengi. Hivyo maendeleo yao yalikuwa polepole wakahitaji chakula kingi kulisha askari pamoja na wapagazi. Askari pamoja na sehemu ya wapagazi walikuwa wageni ambao hawakuzoea vema hali ya hewa na magonjwa hivyo walisumbuliwa kiafya. Kwa mfano kikosi cha 9th South African Infantry ilifika mwezi wa Februari 1916 chenye askari Wazungu 1.135 na hadi Oktoba ni 116 pekee waliobaki tayari kwa vita, ingawa kikosi hiki hakikuona mapigano na idadi yao ilipungua kutokana na magonjwa pekee.

Kinyume chake Lettow Vorbeck aliwategemea hasa askari Waafrika waliokuwa na mahitaji madogo waliojua nchi na kuzoea magonjwa ya mazingira. Waingereza walitumia askari Waafrika hasa kwa kulinda reli ya Uganda kwa sababu mwanzoni walikosa imani katika uwezo wao.                                     

4. Awamu ya tatu: vita ya msituni

Tangu mwaka 1917 Waingereza walipunguza idadi ya Wazungu na Wahindi badala yake waliunda vikosi vipya vya Waafrika vya Kings African Rifles waliokuwa na uwezo wa kushindana na Waafrika wa Lettow Vorbeck.

Walifaulu kusukuma jeshi la Schutztruppe kusini zaidi. Katika Oktoba 1917 waliwalazimisha Wajerumani kusimama kwenye mapigano ya Mahiwa ambako Lettow Vorbeck aliwashinda lakini alipoteza askari mamia. Pia akiba yake ya risasi ilielekea kwisha. Kikosi kikubwa cha askari 1000 chini ya kapteni Tafel walilazimishwa kusalimisha amri baada ya kuishiwa chakula na risasi kabisa. Hata kama hakushindwa, Lettow Vorbeck hakuweza kuendelea vile akaamua kuondoka katika Tanganyika na kwenda Msumbiji alipotegemea Wareno kuwa adui mdhaifu.

                                     

5. Awamu ya nne: Msumbiji na mwisho

Mwisho wa Novemba 1917 Lettow aliwaacha wajeruhiwa na sehemu kubwa ya Wajerumani raia walioongozana naye nyuma akavuka mto Rovuma na askari 280 Wajerumani na Waafrika 1600.

Katika Msumbiji aliweza kuteka kambi ya kijeshi ya Wareno alipokamata bunduki na risasi pamoja na chakula. Waingereza walijaribu kumfuata laini walishindwa kumkuta katika Msumbiji. Katika miezi ya 1918 iliyofuata Lettow Vorbeck alizunguka katika Msumbiji ya kaskazini, mara nyingi kwa umbali wa matembezi ya siku 2 au tatu na Waingereza na Wareno waliomtafuta bila kumpata. Alivamia vituo mbalimbali vya Wareno na kupata risasi na vyakula mara kwa mara.

Katika Septemba 1918 alipata habari ya kwamba Waingereza walikuwa nyuma yake kwa jeshi kubwa. Hapa aliamua kurudi Tanganyika na kuelekea Rhodesia kwa sababu habari zilimfikia ya kwamba Waingereza hawakuwa tena na jeshi huko. Tarehe 28 Septemba alivuka tena mto Rovuma akaendelea katika sehemu za kusini kupitia Songea na Mbozi. Mwezi wa Novemba aliingia Rhodesia ya Kaskazini Zambia. Tarehe 13 Novemba kikosi chake kiliteka mji wa Kasama ambako Waingereza wachache walikimbia walipomwona. Siku iliyofuata afisa Mwingereza alikaribia kambi yake na kumletea habari ya kwamba vita ilikwisha tayari na Ujerumani iliwahi kusimamisha mapigano yote tangu 11 Novemba 1918. Lettow alipatana na Waingereza kuongoza askari hadi mji wa Abercorn leo Mbala, Zambia aliposalimisha amri tarehe 23 Novemba 1918.

                                     

6. Marejeo

 • Anderson, Ross. The Forgotten Front: The East African Campaign: 1914–1918. Tempus Publishing, Ltd. 2004 ISBN 0-752-42344-4
 • Sibley, J.R. Tanganyikan Guerrilla. New York: Ballantine Books. 1973 ISBN 0345098013
 • Abbott, Peter. Armies in East Africa 1914–1918. Osprey, 2002 ISBN 1-841-76489-2
 • Strachan, Hew. The First World War in Africa. Oxford: Oxford University Press. 2004 ISBN 0-199-25728-0
 • Stapleton, Tim. The Rhodesia Native Regiment and the East Africa Campaign of the First World War. Wilfrid Laurier University Press. 2005. ISBN 9780889204980
 • Strachan, Hew. The First World War, To Arms. Oxford addition. 2003. ISBN 978-0199261918
 • Young, F. Brett. "Marching on Tanga." New York: E.F. Dutton & Co. 1917.Medical officers account of campaigning with General Smuts.
 • Crowson, Major Thomas A. When Elephants Clach: A Critical Analysis of Major General Paul Emil von lettow Vorbeck in the East African Theatre of the Great War, 2001 ISBN 0-9540517-0-X
 • Stevenson, William. The Ghosts of Africa. New York: Ballantine Books. 1981 ISBN 0-345-29793-8 fictionalized account
 • Pugu Hadi Peramiho - kimehaririwa na P. Gerold Rupper, OSB, BPNP, Peramiho 1988, ISBN 9967 67 031 1


                                     
 • makoloni hasa Uingereza, Ufaransa na Hispania. Kampeni za Kivita katika Afrika ya Mashariki Vita ya Kwanza ya Dunia American Battle Monuments Commission 1938
 • Kondoa - Irangi Kikosi cha 14.: Mwanza na Ikoma Kampeni za Kivita katika Afrika ya Mashariki Vita ya Kwanza ya Dunia Florian Hoffmann: Okkupation und Militärverwaltung
 • Posidi, mtu wa kwanza kuandika habari za maisha ya Augustino kwa Kilatini, Vita Augustini alisema waamini wanamkuta daima hai katika vitabu vyake
 • Jamhuri ya Kenya ni nchi iliyoko Afrika Mashariki katika ikweta, kando ya Bahari ya Hindi. Kenya imepakana na Ethiopia kaskazini Somalia kaskazini

Users also searched:

...
...
...